Jumatatu 7 Septemba 2026 - 18:18
Ubalozi wa Iran Vatican Wawataka Viongozi wa Dini Kuvunja Ukimya

Hawza/ Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Vatican, kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa kigaidi wa Marekani kusini mwa Iran, katika eneo la Sirik, umewataka wanazuoni, viongozi wa dini na viongozi wa madhehebu yote kuvunja ukimya, na kuifanya mimbari na mihrabu kuwa sauti ya kupaza kilio cha uadilifu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Vatican umetoa taarifa ya kulaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya eneo la Sirik. Maudhui ya taarifa hiyo ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu aliyemheshimu mwanadamu na kuipa heshima na utukufu nafsi yake;

Ni kwa namna gani tunaweza kunyamaza mbele ya umwagwaji damu ya watu wasio na hatia? Tunawezaje kulitaja jina la Mwenyezi Mungu kwa ndimi zetu, kusimama kwa ajili ya ibada na kuzungumzia imani na maadili, huku tusisikie kilio cha akina mama wanaolia juu ya miili ya watoto wao?

Kuwaua wanadamu wasio na ulinzi, hususan wanawake na watoto, katika ardhi yoyote na kwa mkono wa jeshi au mamlaka yoyote ile, ni jinai dhidi ya mwanadamu na uasi dhidi ya heshima ya uhai. Hakuna mamlaka ya kisiasa, hakuna madai ya kiusalama wala maslahi yoyote ya kimaeneo yanayoweza kuifanya damu ya mtu asiye na hatia kuwa halali kumwagwa.

Dini zimekuja ili kuamsha dhamiri ya mwanadamu, si ili zisinzie mbele ya dhuluma. Mitume wa Mwenyezi Mungu wamekuwa watangazaji wa uadilifu, rehema na heshima ya mwanadamu.

Inawezekanaje nyumba kubomolewa juu ya watoto, mama akamtoa mtoto wake kutoka chini ya vifusi, familia ikateketea kwa muda mfupi, na sherehe ya harusi ikageuka kuwa msiba na maombolezo, huku wenye kushikilia mimbari, mihrabu, makanisa, masinagogi na maeneo mengine ya ibada duniani wakiwa watazamaji tu?

Mbele ya Mwenyezi Mungu, damu ya aliyedhulumiwa haihitaji kitambulisho; mtoto aliyeuawa, kabla ya kuwa wa taifa au dini fulani, ni mwanadamu ambaye alikuwa na haki ya kuishi.

Leo, wajibu wa viongozi wa dini ni mzito. Tunawaomba wanazuoni, viongozi wa dini na viongozi wa madhehebu yote kuvunja ukimya. Mimbari na mihrabu inayonyamaza mbele ya damu ya watu waliodhulumiwa, inawezaje kuwaita watu kwenye uadilifu na rehema?

Imani hupata maana pale inapokuwa na msimamo dhidi ya dhuluma, inapomtetea aliyedhulumiwa na inapoiweka heshima ya uhai wa mwanadamu juu ya maslahi ya wenye nguvu.

Enyi viongozi wa dini duniani! Leo, kuliko wakati mwingine wowote, sauti zenu zinapaswa kuwa sauti ya dhamiri ya mwanadamu. Simameni pamoja na, bila kujali masuala ya kisiasa, laanini mauaji ya raia, wanawake na watoto, kuhamishwa watu kutoka katika makazi yao na kuharibiwa nyumba zao.

Ziombeni kwa ujasiri serikali na majeshi ya kigaidi ya Marekani kuacha mauaji ya kikatili na mashambulizi ya kinyama yanayolenga maeneo ya makazi na raia wasio na ulinzi, kuheshimu uhai wa mwanadamu na kujitahidi kusitisha vitendo vya ukatili pamoja na kuwalinda watu wasio na hatia.

Msiruhusu dini itumike kuwa chombo cha kuhalalishia vita; irejesheni dini kuwa lugha ya rehema, uadilifu na hifadhi ya waliodhulumiwa.

Tukumbuke: Siku ambayo hakuna nguvu itakayobaki, hakuna cheo, hakuna bendera wala mipaka, kitakachobaki mbele ya Mwenyezi Mungu ni matendo ya mwanadamu.

Huenda siku hiyo moja ya maswali yenye kutisha zaidi ikawa: “Wakati watu wasio na hatia walipokuwa wakiuawa na watoto wakipoteza maisha chini ya vifusi, wewe ambaye uliweza kuzungumza, kwa nini ulikaa kimya?”

Imani katika Kristo si msalaba tu shingoni, mshumaa kanisani au dua midomoni; imani ni kusimama upande wa mwanadamu anayeteseka, yule mwanadamu ambaye Kristo alituonesha kupitia sura ya mwenye njaa, mgeni, aliyenyimwa haki na aliyedhulumiwa.

Mtoto anapouawa katika vita, si moyo wa mama mmoja tu unaovunjika; ni kana kwamba sehemu ya mwili wa ubinadamu inapelekwa msalabani. Nyumba inapobomolewa juu ya familia, mama anapopaza sauti akilitaja jina la mtoto wake katikati ya vifusi bila kupata jibu, Mkristo hawezi kuuliza: Mtoto huyu alikuwa wa taifa gani, kabila gani au dini gani?

Kristo alitufundisha kwamba “jirani” tusimtafute kwa kuzingatia mipaka ya kabila na dini. Kwa sababu hiyo, mauaji ya raia, wanawake na watoto, yanapofanywa na jeshi au mamlaka yoyote ile na katika kona yoyote duniani, yanapaswa kulaaniwa kwa sauti iliyo wazi na bila kutumia viwango viwili.

Haiwezekani kushika Injili ya upendo mkononi na kunyamaza mbele ya mateso ya mwanadamu. Haiwezekani siku ya Jumapili kuzungumzia upendo kwa jirani, halafu siku nyingine kufumba macho mbele ya vifo vya watoto kwa sababu ya masuala ya kisiasa.

Uhai wa kila mwanadamu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu na una heshima ambayo mamlaka za kidunia hazina haki ya kuinyang’anya. Makanisa ya dunia yangeweza, yakivuka mipaka ya kisiasa na tofauti za kidini, kutangaza kwa sauti moja: Hakuna mtoto ambaye ni adui; hakuna mama anayestahili kuomboleza mtoto wake; na hakuna ushindi unaojengwa juu ya damu ya watu wasio na hatia ambao unaweza kuwa ushindi wa Kristo na Injili.

Na huenda leo swali linalokabili dhamiri ya kila Mkristo likawa ni lile swali la milele la Injili: “Wakati mwanadamu aliyejeruhiwa na anayeteseka amelala kando ya njia, je, tutapita pembeni yake, au kama Msamaria Mwema, tutasimama?”

Kwa sababu Kristo hakutuita tutazame tu mateso ya mwanadamu, bali alituita tumpende; na mbele ya damu ya watu wasio na hatia, upendo wa kweli hauwezi kamwe kunyamaza.

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran – Vatican

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha